Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim
Majaliwa amesema serikali imeunda tume kuchunguza taarifa inayoelezea
utaratibu uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro
kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti
Serengeti.
Tume hiyo pia itatafuta kaburi la faru huyo ambaye inadaiwa alifariki.Amesema timu hiyo ya wataalamu tayari imeshafika Sasakwa VIP Grumet kwa ajili ya kutafuta kaburi na kuchukua vinasaba vya masalia ya faru John.
Baadaye watakwenda kwenye Hifadhi ya
Ngorongoro kuchukua vinasaba vya watoto wake na kuvilinganisha na pembe hiyo ili kubaini kama kweli pembe aliyopelekewa ni ya faru John au la.
"Tume niliyounda kwa ajili ya uchunguzi wa faru John imetua VIP Grumet Serengeti kujiridhisha kama kuna kaburi la faru John na kama lipo wachukue vinasaba. Lengo ni kutaka kubaini kama pembe iliyowasilishwa kwangu Disemba 9 mwaka huu ni ya faru John," Bw Majaliwa alisema akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Bw Majaliwa amesema wakati faru John akiwa V I P Grumet taarifa zilisema ni mgonjwa na daktari alipompima mara ya kwanza akabaini faru huyo hakuwa na ugonjwa wowote.
"Daktari alimpima tena kwa mara ya pili taarifa zikasema tena si mgonjwa ghafla wakasema amekufa. Hili haliwezekani,".
Waziri Mkuu amesema ameiagiza timu hiyo kufanya kazi ya uchunguzi wa taarifa hizo kikamilifu kwa sababu Serikali imetumia fedha nyingi kuwaleta faru hao kutoka nchini Afrika Kusini.
"Ni lazima nyara hizo za Serikali zilindwe kwa manufaa Taifa," alisema.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof Jumanne Maghembe, alipokuwa anawasilisha taarifa ya utaratibu uliotumika kumhamisha faru John wiki mbili zilizopita, alisema hadi kufikia Desemba 2015 wakati faru John anahamishwa alikuwa na watoto 26 - sawa na asilimia 70.2- ya faru wote waliokuwepo ndani ya kreta.
"Uamuzi wa kumuondoa John ulikuwa ni muhimu ili kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la 'inbreeding' ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro," alisema Prof Maghembe.
Alisema baada ya kuhamishiwa Sasakwa, Julai 10, 2016 afya ya faru John ilianza kudorora na alikufa tarehe 18 Agosti, mwaka huu.
Taarifa hiyo iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya Kuwalinda Tembo na Faru ambayo inajumuisha Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Mkurugenzi Mkuu wa NCAA na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Bw Robert Mande alikabidhi Bw Majaliwa pembe za faru John huyo.
Kwa mujibu wa Bw Mande, pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na uzito wa kilo 2.3.
Source BBC Swahili
0 comments:
Post a Comment